#WC2018: Zidane akana kufukuzia ukocha timu ya Taifa Ufaransa

Muktasari:

Zidane aliishtua dunia alipotangaza kuachia ngazi katika klabu ya Real Madrid, siku chache baada kuwaongoza Los Blancos kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo. Tayari nafasi yake imeshachukuliwa baada ya uongozi wa klabu hiyo, kumtangaza kocha Hispania, Julen Lopetegui.

Kocha wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesisitiza kuwa, hana mpango wa kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa, lakini kama Mfaransa yeyote yule, yuko nyuma ya Les Blues, katika michuano ya Kombe la Dunia na anatamani kuiona ikishinda taji kwa mara ya pili.

Zidane aliishtua dunia alipotangaza kuachia ngazi katika klabu ya Real Madrid, siku chache baada kuwaongoza Los Blancos kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo. Tayari nafasi yake imeshachukuliwa baada ya uongozi wa klabu hiyo, kumtangaza kocha Hispania, Julen Lopetegui.

Haraka sana, watu wakaanza kumhusisha, gwiji huyo mwenye umri wa miaka 45 na kazi ya kukinoa kikosi cha timu ya taifa, ambayo ni moja ya timu zinazopigiwa upatu kufanya mambo makubwa nchini Russia. Ufaransa kwa sasa iko chini ya ukufunzi wa Didier Deschamps.

"Eti kuinoa France, nani kasema? Hapana mimi naisapoti ufaransa kama mwananchi wa kawaida, natamani kuona wakitwaa taji hili kwa nyingine tena baada ya mwaka 1998. Hiyo ndio dua ya kila mfaransa sio kuchukua kazi za watu," alisema Zidane.

France wako katika kundi C ambapo wataanza kampeni yao dhidi ya Australia, kabla ya kukabiliana na Peru na Denmark.