VIDEO: Diamond aacha historia safari ya Kigoma
Kigoma. Msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ amefanya tukio litakalobaki vichwani mwa watu baada ya kutumia usafiri wa treni akiwa na wananchi wengine kwenda mkoani Kigoma na kuacha usafiri wake wa kifahari VX.
Kwa kutumia VX, huenda Diamond angetumia saa chache kufika, lakini hakutaka iwe hivyo na kuamua kupanda treni ambayo alitumia zaidi ya siku moja.
Katika safari hiyo, Diamond aliongozana na mashabiki, familia yake akiwemo mtoto wake mdogo pamoja na mzazi mwenzake, Tanasha Dona. Pia alikuwa ameambatana na wasanii kadhaa.
Msanii huyo amesafiri kwenda alikozaliwa mama yake, Sandra kwa lengo la kuwapa shukurani mashabiki kwa kumsapoti katika miaka 10 ya safari yake ya kimuziki.
Akiwa ndani ya treni hiyo iliyoondoka Dar es Salaam, Desemba 27, saa mbili asubuhi, alijichangaya kama vile sio bosi wa watu zaidi ya 50 walioko nyuma yake.
Kwa baadhi ya maeneo ambapo treni hiyo ilipita ikiwemo Morogoro,Dodoma na Tabora, Diamond alisimama na kuwasalimia mashabiki zake wakiwemo vijana, wazee, wanawake na watoto.
Baadhi ya abiria walionekana kufurahia safari hiyo na kusema wamejifunza mambo mbalimbali ambayo waliokuwa hawayafahamu.
Nguruka wavunja rekodi
Katika vituo vyote walivyopita, Stesheni ya Nguruka iliyopo mkoani Kigoma ilivunja rekodi kwa mapokezi ya aina yake.
Katika stesheni hiyo ambayo ni ya kwanza unapoingia mkoani Kigoma, Diamond alikutana na umati mkubwa wa mashabiki wakimsubiri.
Mashabiki wa eneo hilo walitengeneza jukwaa na kujikusanya mithili ya watu waliokuwa wakisubiri mkutano wa hadhara.
Alipowasili saa 8 mchana, Diamond alipanda jukwaani na kuanza kuimba wimbo wa ‘Baba Lao’ ambao ulionekaba kuiteka safari nzima ya Kigama.
Diamond alitumia nafasi hivyo kuwaita wasanii wengine katika jukwaa hilo lililokuwa limepambwa kwa vitambaa ya bluu na nyeupe na kuwekwa zulia jekundu.
Baadhi ya wasanii hao ambao wapo chini ya lebo ya wasafi ni Queen Darleen, Lavalava, Rayvanny na Yong Killer ambaye aliacha maswali huenda naye ni kati ya wasanii wanaotarajia kuwasajili katika lebo hiyo.
Wasanii hao walitumbuiza kwa dakika kadhaa, tukio lililowachukia nusu saa kabla ya kuendelea na safari.
Diamond alitumia nafasi hiyo kuwaomba mashabiki wasikose tamasha litakalofanyika Desemba 31, katika viwanja vya Lake Tanganyika. Pia aliwashukuru kwa mapokezi makubwa waliyomfanyia na kusema hakuyatarajia.
Aliwaahidi mashabiki hao kuwa ataruidi siku nyingine na kuwapa burudani.