Kikapu kanda ya ziwa yapigwa kalenda

Muktasari:

  • Mashindano hayo yanalengo la kupata bingwa wa Kanda ya Ziwa

Mwanza. Mashindano ya mpira wa kikapu ya kusaka bingwa wa mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyokuwa yaanze leo Jumamosi jijini Mwanza, yamepigwa kalenda kwa madai ya baadhi ya mikoa kutothibitisha ushiriki wake.

Kamishna wa ufundi na uendeshaji wa mashindano ya chama cha mpira wa kikapu Mkoa wa Mwanza, (MRBA) Haidar Abdul amesema hadi sasa ni Mkoa wa Mara pekee uliothibitisha, hivyo wanaendelea kuwasiliana na mikoa mingine kujua hatma yao.

Alisema kuwa wanatarajia kesho Jumapili kukaa kikao kujadili lini wataanza mashindano hayo na jumla ya Mikoa itakayoshiriki.

"Tumesogeza mbele mashindano haya na kesho Jumapili ndio tutakaa kupanga tena tarehe na hii imetokana na baadhi ya Mikoa kutothibitisha ushiriki wake, kwahiyo tunaendelea kujipanga" alisema Abdul.

Jumla ya Mikoa mitano yenye timu 10 ilitarajia kushiriki mashindano hayo, ikiwa ni wenyeji Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita na kila mkoa ulipaswa kuwa na timu mbili.