Lampard ataja sababu ya kuifunga Arsenal

Muktasari:
- Kocha wa Chelsea Frank Lampard amesema haikuwa kazi nyepesi kupata ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates.
London, England. Licha ya kupata pointi tatu, Frank Lampard, amesema Chelsea ilicheza ovyo dakika 30 za kipindi cha kwanza.
Kauli ya Lampard imekuja muda mfupi baada ya Chelsea kutoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates.
“Dakika 30 za kipindi cha kwanza tulicheza vibaya, tulitoa nafasi kwa Arsenal wafanye wanavyotaka, lakini walishindwa kutumia vyema fursa hiyo,”alisema kocha huyo.
Mikel Arteta aliyerejea Emirates akiwa kocha baada ya kucheza kwa mafanikio kama nahodha, alifura kwa hasira baada ya Chelsea baada ya kinda Abraham Tammy kufunga bao la pili.
Nahodha Pierre-Emerick Aubameyang alitangulia kuipa bao Arsenal kabla ya timu hiyo kuzidiwa kipindi cha pili na kuruhusu mabao mawili.
Arsenal iliyopata pigo baada ya beki Calum Chambers kuumia kipindi cha kwanza itaingia mwaka mpya ikiwa nyuma pointi 11 dhidi ya Chelsea inayoshika nafasi ya nne katika ligi na haikuwahi kupata ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani tangu Oktoba 6.
Arteta alisema amesikitishwa na matokeo hayo kwa kuwa walicheza vizuri kipindi cha kwanza kabla ya kupoteza mwelekeo dakika 45 za mwisho.
“Tulitumia nguvu kubwa kucheza kwa kujilinda kipindi cha kwanza, unapocheza na timu kama Chelsea unatakuwa kuwa nguvu ya kutosha, tunapaswa kuhimili vipindi vyote,”alisema Arteta.