MAONI YA MHARIRI: Mamlaka haya ya Ma-RC, DC yarekebishwe

Rais John Magufuli

Muktasari:

Huu ni mwendelezo wa maagizo mengi ya wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka rumande watu wanaotofautiana nao katika shughuli na baada ya kulala siku moja ndani huwaachia bila ya kuwafikisha mahakamani.

Kwenye toleo letu la jana, ukurasa wa tatu kulikuwa na habari inayohusu agizo la mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuwasweka ndani madiwani wanne wa Chadema kwa madai kuwa wanakwamisha utekelezaji wa kazi zake. Mkuu huyo wa wilaya anadai kuwa madiwani hao wamekuwa wakipotosha umma kuhusu ziara zake na kuwaeleza wananchi kinyume chake.

Huu ni mwendelezo wa maagizo mengi ya wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka rumande watu wanaotofautiana nao katika shughuli na baada ya kulala siku moja ndani huwaachia bila ya kuwafikisha mahakamani.

Vitendo hivyo ni utekelezaji wa Sheria ya Wakuu wa Mikoa ya mwaka 1962 na ya Wakuu wa Wilaya ya mwaka 1962 na Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 ambazo zinawapa viongozi hao mamlaka ya kumuweka mahabusu mtu yeyote kwa saa 48 iwapo wataona anaweza kuvunja amani au kuvuruga utulivu uliopo na kwamba vitendo hivyo haviwezi kudhibitiwa isipokuwa kwa kumuweka ndani mtu huyo.

Sheria hiyo inasema kuwa iwapo itatokea hivyo, yaani mwananchi atawekwa ndani kwa kutumia sheria hiyo, mtu huyo anatakiwa afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 baada ya kukamatwa na kuwekwa ndani na isipofanyika hivyo, mtu huyo aachiwe huru na asikamatwe tena kwa kosa hilo hilo kwa kutumia mamlaka ya sheria hiyo.

Hizi ni kati ya sheria ambazo Tume ya Jaji Francis Nyalali iliziona kuwa zinakiuka katiba na pia kutumiwa vibaya na waliopewa mamlaka hayo. Na katika ulimwengu huu, unaweza kusema sheria hizo zimepitwa na wakati.

Moja ya sababu zilizotolewa na Tume ya Jaji Nyalali ni ukweli kwamba kati ya watuhumiwa wa kuvuruga amani na utulivu ni wasumbufu wa kisiasa na wananchi wanaopinga miradi binafsi.

Kwa maoni yake, mkuu wa mkoa au wilaya anaweza kuchukulia kitendo cha mwanasiasa kuelimisha wananchi waliomchagua kuhusu mipango inayotekelezwa na Serikali au mkuu huyo, kuwa ni kuwashawishi wasikubaliane na utekelezwaji huo na hivyo kuchukulia kuwa mwanasiasa huyo anaweza kuvuruga amani na utulivu na hivyo kuamua akamatwe na kuwekwa ndani.

Na kwa kuwa sheria inampa saa 48 awe amemfikisha mahakamani au kumuachia bila ya kumkamata tena, mkuu huyo anaweza asimfikishe mahakamani na akaamua kumuachia kwa kuwa sheria imempa mwanya huo.

Tunadhani kuwa kama Tume ya Jaji Nyalali ilivyoona kuwa sheria hiyo haifai na hivyo ifutwe au irekebishwe, kuna haja ya kufanya hivyo mapema kwa kuwa inaonekana badala ya makusudio yaliyokusudiwa, matumizi ya sheria hii yanaweza kuwa mabaya kiasi cha kuweza kuanza kujenga chuki baina ya wanaiokamatwa kwa amri hizo na viongozi wao na baadaye chuki hiyo kuenea.

Hakuna tatizo kwa viongozi hao wa mikoa na wilaya kuwa na mamlaka hayo, lakini kama Tume ya Jaji Nyalali ilivyosema kuna haja ya kuweka utaratibu wa haki ya kumpa haki mtu anayewekwa ndani kimakosa au kwa uonevu, kupinga kitendo hicho kwenye vyombo vya kisheria ili kuwafanya waliopewa mamlaka hayo kuitumia sheria kwa uangalifu na bila uonevu.

Kuendelea kuwaachia mamlaka hayo makubwa ya kuwaweka ndani wananchi bila ya kuwawekea utaratibu wa kulazimika kuwajibika kwa vitendo vyao, kunatoa mwanya kwa viongozi hao kufanya vyovyote watakavyo kwa kutumia suala la amani na utulivu. Ni miaka mingi tangu Tume ya Nyalali ilipoibua hoja hizo na hivyo tunadhani wakati muafaka umefika wa kufanyia kazi mapendekezo yake.